Tarehe 28 Julai 2025 kundi la madereva 28 wa Kitanzania, kati ya madereva 103 wa kundi la kwanza, limewasili katika Jiji la Doha tayari kuanza kazi zao katika Kampuni ya Mowasalat Karwa. Madereva hao ni sehemu ya jumla ya madereva 447 wa Kitanzania waliopata nafasi ya ajira kupitia mchakato wa usaili uliofanyika siku za hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
Madereva hao waliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Hamad na kupokelewa rasmi na Uongozi wa Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Qatar, ukiongozwa na Mkuu wa Utawala, Bibi Maryam H. Mrisho, kwa niaba ya Mhe. Habibu Awesi Mohamed Balozi wa Tanzania nchini Qatar. Aidha, walipokelewa pia na wawakilishi wengine kutoka Ubalozi wa Tanzania nchini Qatar na menejimenti ya Kampuni ya Mowasalat Karwa.
Akizungumza wakati wa mapokezi, Bibi Maryam aliwasihi madereva hao kuwa watulivu, watii sheria na masharti ya ajira, waonyeshe weledi, nidhamu, na uvumilivu katika utoaji wa huduma za usafirishaji nchini Qatar, ikizingatiwa kuwa wao ni mabalozi wa Tanzania kupitia kazi yao.
Makundi mengine ya madereva waliobaki katika kundi la kwanza yanatarajiwa kuwasili nchini Qatar kati ya tarehe 29 hadi 30 Julai 2025, na kuhitimishwa kati ya tarehe 1 hadi 3 Agosti 2025, kukamilisha idadi ya madereva 103 wa awamu ya kwanza
Kwa upande mwingine, maandalizi ya kuwasili kwa makundi mengine ili kufikisha idadi kamili ya madereva 447 yataendelea mara tu taratibu za upatikanaji wa Visa na tiketi za usafiri zitakapokamilika.
Ubalozi wa Tanzania nchini Qatar unaendelea kushirikiana kwa karibu na mamlaka husika kuhakikisha mazingira bora ya kazi na ustawi wa Watanzania wote wanaofanya kazi katika nchi hiyo.
