Doha, Qatar – Kuanzia tarehe 29 Juni hadi 03 Julai 2025, Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Qatar uliratibu ziara muhimu ya wafanyabiashara wadogo na wa kati kutoka Tanzania. Makampuni Kumi na moja (11) ya Kitanzania yaliyoshiriki katika ziara hiyo ni pamoja na:
Leenez General Trading, Fortuna Legacy Company Ltd, Agropro Solutions Ltd, Maglis Trading, Spine Company Ltd, Afrisoko Export and Import, Savez International Company Ltd, Nanine Business Enterprises Co. Ltd, Highlands Organic Co. Ltd, Alabama Trading Company and Hotfirm Enterprises Limited.
Ziara hiyo ilifanyika jijini Doha na ilihusisha mikutano ya ana kwa ana kati ya wafanyabiashara wa Tanzania na wenzao wa Qatar, ikiwa na lengo la kuimarisha ushirikiano wa kibiashara, kubadilishana uzoefu, na kutafuta fursa za kiuchumi katika soko la kimataifa.
Lengo kuu la ziara hii lilikuwa kuimarisha uhusiano wa kibiashara kati ya Tanzania na Qatar sambamba na kuweka msingi wa ushirikiano wa kudumu kati ya wafanyabiashara wa pande zote mbili. Aidha, ziara hii imelenga:
• Kutangaza bidhaa na huduma zinazozalishwa na wajasiriamali wa Tanzania, hasa katika sekta za kilimo, mifugo, na maliasili;
• Kutafuta fursa mpya za masoko ya bidhaa za Kitanzania katika soko la Qatar na Mashariki ya Kati kwa ujumla;
• Kuongeza mtandao wa mawasiliano ya kibiashara (networking);
• Kuwavutia wabia wa biashara na wawekezaji wa kimataifa kushirikiana na wafanyabiashara wa Tanzania.
Katika kipindi cha ziara hiyo, wafanyabiashara wa Tanzania walipata fursa ya kukutana na kufanya mazungumzo ya kibiashara na kampuni mbalimbali nchini Qatar, zikiwemo:
World Fruits Centre W.L.L; BRACO Trading L.L.C; United Group of Company; Kathmandu Trading and Contracting W.W.L; Safari Hypermarket; Versa Trading and Catering; East Africa Coffee Management – Doha; ADK Food Company; Al Mutasaliq Trading Centre; Freight Link and Logistics; Family Hypermarkets; Arkan Alarab Sunflower Oil Company; Lulu Hypermarkets; Ansary Gallery Hypermarket; na Smart Outsourcing Solution for Trading (SoS).
Matokeo ya ziara hiyo ni pamoja na:
• Makampuni sita (06) ya Kitanzania yamesaini Hati ya Makubaliano ya kuuza kahawa (coffee beans) na kampuni ya East Africa Coffee ya nchini Qatar;
• Makampuni tisa (09) ya Kitanzania yamepokea Barua ya Makubaliano ya Awali (Letter of Intent) pamoja na Oda za Ununuzi (Purchase Orders) kutoka kampuni ya chakula ya ADK – Doha, ambapo sampuli za bidhaa ya Ufuta (Sesame) zenye uzito wa tani 40 zinatarajiwa kuwasilishwa nchini Qatar mapema mwezi Julai 2025 kwa ajili ya kuidhinishwa kwa oda kamili;
• Makampuni nane (08) kutoka Tanzania kupata mikataba ya kuiuzia kampuni ya Kathmandu Trading and Contracting W.W.L ya nchini Qatar nyama ya ng’ombe, mbuzi, kondoo na bidhaa nyekundu za tumboni kwa kipindi cha kati ya miezi sita hadi mwaka mmoja.
Aidha, baadhi ya kampuni nyingine za Qatar zimeonesha nia ya kuendelea na mazungumzo ya kibiashara na kuomba kuwasilishwa mapendekezo ya bei za bidhaa kutoka kwa wafanyabiashara wa Tanzania, ikiwa ni hatua nyingine ya kuendeleza ushirikiano wa kibiashara kati ya nchi hizi mbili.
Ubalozi wa Tanzania nchini Qatar unapongeza juhudi kubwa zilizofanywa na wafanyabiashara waliohudhuria kwa kuonesha uzalendo, ubunifu, na dhamira ya kuendeleza uchumi wa Taifa kupitia biashara ya kimataifa. Vilevile, unatoa wito kwa wadau wengine kuendelea kushirikiana na kutumia majukwaa ya kimataifa kama haya katika kufungua fursa mpya za kiuchumi kwa Tanzania.











