12/02/2025

Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Qatar, Mheshimiwa Habibu Awesi Mohamed amehudhuria hafla ya utiaji saini wa Hati ya Makubaliano  (MoU) kati ya Kampuni ya Dream and Guide Hospitality ya Qatar na Kampuni ya usambazaji nyama ya Tanzania ya WRIS Agro Company Limited.
Makubaliano hayo yanajikita katika usambazaji wa nyama iliyogandishwa ya mbuzi, ng’ombe, na kondoo na bidhaa za viungo vya ndani vya mifugo hiyo.
Kusainiwa mwa MoU hiyo ni matokeo ya moja kwa moja ya ushiriki wa Kampuni ya WRIS Agro katika Maonesho ya 12 ya Kimataifa ya Kilimo (AGRITEQ 2025), yaliyofanyika Doha, Qatar, tarehe 4-8 Februari, 2025. 
Kampuni ya WRIS Agro ilitumia maonesho hayo kama jukwaa la kutangaza bidhaa zake za nyama bora na kuanzisha mahusiano muhimu ya kibiashara katika Mashariki ya Kati. 
Ushirikiano na Kampuni ya Dream and Guide Hospitality ni hatua ya kuonesha ongezeko la mahitaji ya nyama baridi na iliyogandishwa yenye ubora wa juu nchini Qatar.
Balozi Awesi ameelezea kuridhishwa kwake na ushirikiano huo na kubainisha kuwa unadhihirisha umuhimu wa maonesho ya kibiashara katika kukuza uhusiano wa biashara kimataifa. 
“Makubaliano haya ni ushuhuda wa mafanikio yanayotokana na ushiriki wa WRIS Agro Company katika Maonesho ya Kilimo ya Qatar 2025 na kuendelea kuimarika kwa uhusiano kati ya Tanzania na Qatar,” alisema Mhe. Balozi Awesi.
Makubaliano hayo mapya yanatarajiwa kufungua fursa zaidi za ushirikiano na kunufaisha sekta za kilimo na biashara za nchi zote mbili na kuhakikisha upatikanaji wa nyama bora katika soko la Qatar.