Baada ya maulizo mengi kuhusu utoaji wa Pasipoti Mpya, ufuatao ni utaratibu wa kushughulikia zoezi hilo katika nchi za uwakilishi wetu*:

A. KUNUNUA FOMU

  1. Mwombaji anaweza kuja Ubalozini na pasipoti aliyonayo ili kununua fomu au atume Euro 10,- (malipo ya fomu kwa rejista) pamoja na kopi mbili za pasipoti aliyonayo kurasa za 1 hadi 5 na ukurasa wa mwisho wenye DN. Namba. Aidha, alete bahasha yenye anuani yake iliyobandikwa stampu za rejista ili apelekewe fomu.
  2. Malipo yakipokelewa, mwombaji atapewa fomu au atapelekewa fomu husika ambayo ataijaza BILA kuweka sahihi yake katika sehemu ya sahihi, ukurasa wa kwanza. Mwombaji ataileta fomu yake, `photocopy' ya fomu iliyojazwa na picha tano (5) za pasipoti saizi ya 4 x 4.5 cm zenye `background' ya rangi ya `sky blue' au rangi ya maji ya bahari. Picha hizo lazima ziwe za karibuni sana zinazoonyesha masikio yote mawili.
    *FOMU IJAZWE KWA HERUFI KUBWA!
  3. a) Wakati wa kujaza fomu `Section 2' tarehe, mwezi na mwaka wa kuzaliwa wazazi ni LAZIMA. Hata wazazi waliofariki.

    b) Kama kuna sababu ya kubadilisha jina lazima hati husika za sababu ya kubadili jina ziletwe - k.m. cheti cha ndoa.

    c) Kama pasipoti imepotea LAZIMA ripoti ya polisi na `affidavit' (hati ya kiapo) mbele ya mwanasheria zitumwe pamoja na fomu.

    Wale watakaopenda kuja Ubalozini kununua fomu na kurudisha fomu wazingatie utaratibu ulioelezwa (1 - 3).

    d) Acha au usijaze kipengele cha sita (6) katika fomu kwa kuzingatia Maelezo Muhimu kwenye kipengele cha pili (2) - waliotajwa hawapatikani nje ya Tanzania.

    e) Kila fomu ina namba moja haitumiki kwa watu wawili. Mwombaji asithubutu kutoa nakala (photocopy) ili itumike kwa mwombaji mwingine.

  4. Inatahadharishwa kuwa fomu za uombaji pasipoti zilizokosewa au kufutwafutwa hazitakubalika itabidi mwombaji anunue fomu nyingine. Ni vema kabla ya kujaza fomu mwombaji atoe nakala (photocopy) ya fomu aijaze kwanza kila kipengele ili baadaye anakili katika fomu aliyopelekewa kuepuka makosa, kufutwafutwa na kununua fomu nyingine.

B. ALAMA ZA VIDOLE NA TAHADHARI

  1. Katika utoaji wa pasipoti mpya lazima mwombaji achukuliwe alama za vidole (`finger prints') na kuweka sahihi kwa mkono wake mwenyewe mbele ya afisa mhusika. Hivyo, tarehe ya kuchukuliwa alama za vidole; mwombaji atajulishwa kwa simu au e-mail.
  2. Mwombaji LAZIMA aje UBALOZINI ili kutia sahihi fomu na kuchukuliwa alama za vidole. Mwombaji atatakiwa alipe Euro 40,- malipo ya pasipoti mpya.
  3. Maombi yatashughulikiwa ipasavyo na kupelekwa haraka Makao Makuu ya Uhamiaji Dar es Salaam katika mfuko maalum wa Kidiplomasia.
  4. Pasipoti mpya zitatolewa Makao Makuu ya Uhamiaji, Dar es Salaam na zitaletwa Ubalozini kwa mfuko maalum.
  5. Ubalozi utatuma pasipoti mpya kwa mwombaji kwa kutumia bahasha iliyoandikwa anuani na mwombaji na kuwekwa stampu za rejista. Pasipoti ya zamani itabidi iwe ´cancelled' ili nayo irudishwe kwa Mwombaji katika bahasha moja na pasipoti mpya. Hivyo, mawasiliano na Ubalozi ni muhimu kwani pasipoti mpya haitatolewa kabla ya zamani kuwa `cancelled'. Watakaotaka kufuata pasipoti zao wenyewe ni ruksa.
  6. Utaratibu mzima wa kushughulikia unatazamiwa kuchukua wiki sita (6) au zaidi. Jumla ya gharama ni Euro 50,- yaani Euro 10,- za fomu na Euro 40,- pasipoti.