Kampuni ya Usafirishaji ya Mowasalat (Karwa) kwa kushirikiana na Kampuni za Mawakala wa Ajira kutoka Tanzania na Qatar, imeanza rasmi zoezi la usahili kwa madereva 800 wa magari makubwa na mabasi, utakaofanyika kuanzia tarehe 27 hadi 30 Mei, 2025 katika Chuo cha Usafirishaji cha Taifa (NIT), kilichopo Mabibo, Dar es Salaam.
Zoezi hili ni sehemu ya jitihada za kuwapata madereva wa Kitanzania watakaokwenda kufanya kazi nchini Qatar kupitia mpango maalum ulioratibiwa na Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mjini Doha chini ya uongozi wa Mhe. Balozi Habibu Awesi Mohamed. Ushirikiano huu umeleta fursa kubwa kwa Watanzania kuingia kwenye soko la ajira la kimataifa, hasa katika sekta ya usafirishaji nchini Qatar.
Vilevile, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Kampuni ya Mowasalat (Karwa) wanatarajia kuanzisha Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) katika maeneo ya Mafunzo ya udereva, ufundi na usafirishaji kwa vijana wa Kitanzania. Makubaliano hayo yatatekelezwa kupitia ushirikiano baina ya Chuo cha Mafunzo cha Karwa – Qatar na Vyuo vya Tanzania ambavyo ni Chuo cha Usafirishaji cha Taifa (NIT), Chuo cha Mafunzo ya Ufundi (VETA) na Chuo cha Karume – Zanzibar. Lengo kuu ni kuongeza ujuzi, kuongeza ajira na kuandaa vijana kwa soko la kimataifa, hasa Qatar katika sekta ya usafiri na usafirishaji.
Usahili umeandaliwa kwa utaratibu maalum uliogawanywa katika makundi manne. Tarehe 27 Mei 2025, usahili utaanza chini ya uratibu wa Kampuni ya Sassy Solutions kwa upande wa Tanzania pamoja na Kampuni ya Ajira ya Waha kutoka Qatar. Kampuni nyingine za Tanzania zitakazoratibu usahili katika siku zinazofuata ni Mkapa Foundation, Larali, na Connect. Zoezi la usahili litajumuisha vipengele viwili muhimu:
1. Mtihani wa kuandika (theoretical test)
2. Mtihani wa vitendo (practical test) ambapo waombaji wataendesha magari husika barabarani.
Mwitikio wa waombaji umeelezwa kuwa mkubwa na vijana wengi wa Kitanzania wamejitokeza chuoni hapo kwa ajili ya kushiriki usahili huo. Zoezi linaendelea kwa mafanikio, likiwa na matumaini makubwa ya kutoa fursa ya ajira kwa vijana wengi, sambamba na kukuza uhusiano wa ajira kati ya Tanzania na Qatar.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kufuatilia kwa karibu mchakato huu na inatoa pongezi kwa Mawakala wa Ajira wa Kitanzania na wale wa Qatar walioshiriki kwa namna ya kipekee katika kuhakikisha uteuzi unafanyika kwa umakini mkubwa.




